News
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amepokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali dhidi ya viongozi wa kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania waliosimamishwa kazi Mei 8 mwaka huu.
Mhe. Ndumbaro amepokea taarifa hiyo Agosti 7, 2024 Jijini Dar es Salaam kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Christopher Kamugisha ambaye ameeleza kuwa Kamati hiyo imebaini dosari 13 kutoka kwa uongozi wa kamisheni uliosimamishwa ikiwemo ya kukosekana kwa mikataba zaidi ya 170 ya baadhi ya mabondia katika mapambano ya ndani na nje ya nchi na kukosekana kwa vielelezo vya matumizi ya fedha shilingi milioni 182.
Kufuatia dosari hizo Mhe. Ndumbaro ametoa siku saba kwa watuhumiwa hao kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wawasilishe nakala za mikataba ya mabondia hao katika ofisi ya Waziri huku akimuelekeza msajili wa vyama vya michezo nchini kuchukua hatua stahiki kufuatia taarifa hiyo.
Aidha, kamati hiyo imetoa mapendekezo sita yakiwemo ya kufanyiwa marekebisho kwa muundo wa kamisheni hiyo, kuangaliwa upya kwa kiwango cha elimu ya uongozi wa kamisheni, katiba na kanuni za kamisheni na vyama shiriki ili zifanyiwe marekebisho kuondoa migogoro isiyo ya lazima.
Kamati hiyo imetoa pendekezo la kuanzishwa kwa mfumo wa kielekitroniki utakaounganishwa na benki ili kuwe na uwazi katika makusanyo na malipo yanayofanywa na kamisheni hiyo sambamba na taarifa za mapato na matumizi kuwasilishwa BMT kila robo ya mwaka.
Aidha, uongozi huo wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa umeongezewa muda wa siku 90 za kufanyia kazi baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya uchunguzi.