News
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amewaomba wadau wa michezo kutoka Brazil kufungua ofisi nchini Tanzania ili kutoa huduma ya michezo ikiwezo ujuzi, utalaamu na mawazo ya kuviendeleza vipaji kwa karibu zaidi.
Mhe. Ndumbaro ameyasema hayo Septemba 04, 2024 alipokutana na kufanya mazungumzo na wadau wa michezo kutoka nchini Brazili waliokuja Tanzania kwa lengo la kuzungumza na wadau wa sekta ya michezo ikiwemo Serikali na vyama vya michezo kuhusu ushirikiano katika sekta hiyo hususani katika mchezo wa soka na riadha.
"Brazil wamepiga hatua sana katika michezo kwa hiyo wamekuja kukaa nasi ili tushirikiane nao nasi tupige hatua kama wao, tumekubaliana tudumishe mahusiano katika nchi hizi mbili," alisema na kuongeza kuwa amewashauri wafungue ofisi nchini Tanzania ili waweze kutoa huduma za kimichezo kwa karibu zaidi.
Hata hivyo, Dkt. Ndumbaro amemshukuru Balozi wa Tanzania nchini Brazil Prof. Adelardus Lubango Kilangi kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaleta wadau hao wakubwa wa maendeleo ya michezo hapa nchini.
"Hawa ndio aina ya Mabolozi ambao Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawataka wawepo na wafanye kazi kama hizi"
Kwa upande wake Balozi Kilangi ameishukuru Serikali kupitia Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mapokezi mazuri akieleza kuwa mazungumzo yaliyofanyika kati ya Serikali na wadau hao wa sekta ya michezo nchini Brazil yatazaa matunda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF) Walles Karia na Mwanariadha mkongwe nchini Tanzania Kanali Mstaafu Juma Ikangaa wamemshukuru Balozi na Serikali kwa ugeni huo wenye tija kwa maendeleo ya michezo nchini wakiahidi kutoa ushirikiano kwa ugeni huo katika vikao vitakavyofanyika kabla kurejea Brazil.
Ujumbe huo uliongozwa na Balozi Kilangi, Luciana Teixeira Silva
Mkurugenzi na Mkuu wa msafara kutoka kampuni ya LTS, Douglas Júlio de Almeida Silva
Mkurugenzi wa kampuni ya LTS , Fernando André da Silva Costa
Mkurugenzi wa Michezo na Masoko wa Wizara ya Michezo nchini Brazil, Paulo Rogério Gaspar Araújo mtaalam wa vipaji wa Ceuzeiro',
Constantino Novais da Silva Barbosa, Rais wa wa Ligi ya Northeast na mshauri masuala ya michezo Rodrigo Guimarães da Fonseca Antonio.