News

Posted On:: Sep, 04 2024
News Images

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema wizara hiyo inakamilisha Katiba ya mfano kwa ajili ya vyama na mashirikisho ya michezo itakayokabidhiwa Oktoba 1, 2024 akivitaka vyama na mashirikisho hayo yajiandae kufuata Katiba hiyo katika kuandaa Katiba zao.

Mhe. Ndumbaro amesema hayo Septemba 3, 2024 Mtumba Jijini Dodoma wakati wa kikao cha kufanya tathimini ya mashindano ya Olimpiki 2024 kilichohusisha vyama vya michezo vilivyoshiriki mashindano hayo, Jijini Paris Ufaransa Julai, 2024 ambavyo ni ngumi, Judo, riadha na kuogelea.

"Mwezi ujao tutazindua mwongozo wa namna ya kushirikiana kati ya Serikali, vyama na mashirikisho, kuwe na utaratibu na mwongozo wa matumizi bora na uwazi ya fedha za vyama vya michezo, kujua mipaka na majukumu ya Wakala, viongozi, meneja na mchezaji katika michezo mbalimbali" amesema Mhe. Ndumbaro.

Amevitaka vyama hivyo kutafuta wachezaji wenye asili ya Tanzania ili waje kucheza nchini pamoja na kufanya ufuatiliaji wa kusaka waachezaji wenye asili ya Tanzania wanaofanya vizuri nje ya nchi watakaotumika katika michezo mbalimbali ya kimataifa.

Aidha, amewataka wawe na mkakati wa kuibua na kuendeleza vipaji, akieleza kuwa Serikali inajenga hosteli na Akademia ya Taifa ya Michezo katika Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya ambapo pamoja na kutoa elimu ya michezo kitakua na uwezo wa kupokea wataalam kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kufundisha wataalam wazawa.

Kwa upande wake Naibu Waziri akizungumza wakati akihitimisha kikao hicho amewataka viongozi hao wahakikishe kila wanachofanya kina matokeo chanya kwa jamii hasa katika kukuza michezo.

Wakichangia kwa nyakati tofauti wajumbe kutoka vyama hivyo, wameishukuru Serikali kwa miongozo na uratibu inaoutoa katika michezo wakisisitiza kuendelea kuongeza ushirikiano kwa Serikali katika kuendeleza michezo kabla ya kushiriki michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi.